Hii ni
makala yangu iliyotolewa leo
Oktoba 8, 2016 kwenye gazeti la
TanzaniaDaima, kama hukupata nakala yako na kwa kukujali msomaji wa
petermmbaga.blogspot.com isome hapa kwa utulivu.
Na
PETER MMBAGA, UDSM(SJMC)
“Ukitaka kumfuga chatu, uandae unga wa kumlisha” hiyo ni kauli ya “kijana wa zamani” kwenye kijiwe
kimoja nikiwa kwenye harakati za kumng’ojea mgeni wangu kituo cha daladala mida ya jioni baada ya jua kunipiga vilivyo mchana wake, nikamuuliza
“kijana wa zamani” unamaanisha nini?
Akanambia kijana huelewi nini? Mimi nina elimu ya
mkoloni nayo inanipa nguvu kudadavuadavua yaliyomo kidogo, Je, wewe vipi?
Nikamwambia nijibu basi “mzee kijana” akasema “homu weki” hiyo, wakati
natafakari kabla mzee hajatoa hoja ya
msingi juu ya maana ya msemo wake, ndipo stori kijiweni zikazidi kunoga, kuna
mshikaji moja akazungumza kuhusu UKUTA(akimaanisha
operesheni ya CHADEMA) aliyotakiwa kufanyika
septemba mosi ikasogezwa tena oktoba mosi kisha kuahirishwa kwa mara nyingine.
Jamaa mmoja akadai hawa maCHADEMA nao wamezidi kila kitu wanahisi
wanaonewa, mwacheni ndugu Magu(Rais John
Magufuli) apige kazi bwana! Mzee tunayemwita “mzee wa busara” akajibu hii ni kizungumkuti kila mtu anavutia
kwake ila serikali iwe makini kwa kauli ya rais kusema hakuna siasa mpaka 2020, sasa kazi ya vyama vya siasa ni
nini?
Kuna mvutano wa CUF na Profesa Ibrahimu Lipumba
nikawa nawaza kichwani mwangu wakati huohuo kuna mbasi akaja na
akatusikilizisha sauti ya Rais JPM juu
ya kuhamia Dodoma. Kwa hisia kidogo akataja kuwa haiwezekani baba wa Taifa
mwalimu Nyerere alisema makao makuu ni Dodoma hivyo kupinga”.
Mzee anayeuza kahawa akasema naona mmedakwa na
kuhamia Dodoma, Yule mleta hadithi za Dodoma akasema “Bongo iliitwa Tanzania
kila kitu kilipatikana hapa, get ready with dom” akatia na umombo kwa mbwembwe kidogo, tukacheka sana!
Uchumi wa Tanzania, au uwepo wa Tanzania unahitaji
kutegemeana ili kumvusha mama Tanzania kwenye lindi la umaskini, sasa wakati
ninawaza hilo mulemule jamaa mmoja akasema “mgawanyiko wa kiuchumi na
kiutendaji unabidi uguse nchi nzima”, serikali si inahama yote bwana!
Tukashindwa kuelewa anamaanisha nini? Akasema ule mlundikano
wa wizara hapa Dar, au ukipita mtaa wa Magogoni unaona nini? Tukashangaa,
nikamuuliza kwani tatizo ni nini?
Akanijibu “Mbasi nawe unaonekana huoni mbali, mimi
naona tugawe wizara hata kimkoa au
kikanda hivi kama Arusha ndiyo kitivo cha utalii Tanzania, ni vema Wizara hata
ikawa pale, haya maswala ya bandari na usafirishaji wa maji ukaa “centre” ya
mikoa husika kama Dar, Tanga na Mtwara”
Mzee mkongwe akasema ni wazo zuri lakini mbona
kwenye ofisi za mkoa ama wizara, ofisi ndogo za mkoa zipo hizo ofisi hata nchi zilizoendelea
sidhani kama zina kitu kama hicho! Mbasi mmoja akasema hiyo haitoshi ila ili
kuweka mgawanyo wa kiserikali, ili “decentralization” ya serikali za mitaa
mpaka serikali kuu hawafiki vyema, hii ni sera ya kibunifu!
Mzee kijana akasema enzi hizo kwenye historia ya utawala wa Mwingireza kama vijana mnasoma, Idara za serikali zilikuwa hazipo mikoani na
wakuu wa Idara hawakutaka kuhama Dar, mchakato wa kupata sehemu tulivu ya mji
mkuu mpaka kufika mwishoni mwa mwaka 1920, Idara ya kilimo na ofisi ya mkuu wa
mkoa wa Mashariki zilihamia Morogoro, Idara ya mifugo ilikwenda Mpwapwa sasa
je, kwa mgawanyo huo tu wa kipindi hicho wizara haziwezekani kweli? Tukajiumauma
tukijibu “inawezekana mzee, eeh inawezakana mzee ila kwa mipango”
Kuna jamaa akatoa nje mada kidogo akadai “ving’ora
viletavyo foleni vitapungua jijini bora waende dom”, tukamshangaa nikajiuliza
hivi foleni Dar kumbe inachangiwa na misafara ya hawa waheshimiwa, nikacheka
kidogo!
Wakati kahawa inaendelea kuchemshwa mzee wa kahawa
akasema “nasikia wakuu wanaharakisha uboreshwaji wa hadhi ya kimataifa hata kwa viwanja vya ndege Dodoma kurahisisha
usafiri na hata mdege umeshuka juzi toka
Kanada”, kuna mfanyakazi mmoja wa benki
akadai mbona ukarabati wa uwanja Dar
unafanyika pia, hapo hakuna hoja labda useme fursa gani zimekwepo baada ya
uwepo wa uwanja mkubwa wa Dar, ajira zimetoka na zitakazotoka kwa upanuzi
unaoendelea.
Jamaa mmoja akanena “hapa Bongo hawajapaendeleza
kivile, nadhani wangepaendeleza Dodoma vyema na nchi kiujumla hata kama wazo ni
la tangu uhuru kuhusu kuhama, je, mikakati waliyoanza nayo kwa awamu zilizopita
ikoje? Nikamjibu jibu la swali kwa swali
“kuhusu miundombinu kiujumla eeeh?”
Yule jamaa wa benki akamjibu “umefanya utafiti kuwa
hawajajiandaa vyema, utafiti mbele ndipo ukosoe”, akabaki tunashangaa, asijue
la kujibu!
Nikamuuliza mzee kahawa vipi? Akajibu piga domo
kwanza, ndipo nikauliza hivi huo uchumi mnaozungumzia mipango miji
inaridhishaje? Mzee wa kahawa akadakia akasema walicho “bugi” muda mrefu Dar
haikuwa na mipango miji, na mimi nkamropokea “kazania kahawa wewe”
Mshikaji mmoja akajibu “mzee kaongea bonge la hoja
wewe, mipango mikakati hamna jiulize wazo dogo la kujenga hata “hoteli” ya
nyota kadhaa pale jirani na uwanja wa ndege wa J.K Nyerere ili kupambana na ajira, pato la taifa, foleni pamoja na muda kwa wasafiri hilo haliwaziki kabisa, hii ndio Tanzania”
Aliposema foleni nikamkumbuka mbasi wangu mmoja
aliyenieleza habari za semina moja aliyohudhuria katika hoteli ya Blue Pearl,
moja kati ya wasemaji wa hiyo semina alizungumzia hali ya foleni ya Bongo
aliyodai inavyosikitisha kwani haiwezekani atoke Afrika kusini kuja Tanzania
kwa masaa matatu na kutoka uwanja wa ndege J.K Nyerere mpaka Blue Pearl kwa
masaa hayohayo matatu, akastaajabu! Ila sisi hatukustaajabu ndio huku “kwetu”
kulivyo!
Mzee wa busara akasema nasikitika pale “nkulu” akimaanisha Ikulu, hata mashujaa
wetu hawathaminiwi hata kwa kumbukumbu angalia, anwani ya nkulu wanaandika
barabara ya “Barack Obama” hivi hata kuiita bararaba ya
Mangi Marealle, Kinjekitie Ngwale au Mirambo. Kuna jamaa muuza chips
jirani kwanye kibanda kilichoandikwa
“Hapa Kazi Tu chips” akasema wakihamia
kuna barabara inaweza kuitwa barabara ya
“George Bush”. Nikamjibu kwa mbwembwe za
kimombo “are you serious”. Akanijibu hapa Dar mbona imewezekana?
Kahawa ikawa tayari tukaanza kunywa uchungu wa
kichangamsha mwili kile, ndipo jamaa
yetu wa bodaboda akatokea akisema hii hela
kutonekana mwisho wake ni nini? “Mzee
kijana” akadakia akisema kila sehemu
hakuna hela halafu eti majipu yametumbuliwa pesa iko wapi?
Yule jamaa wa benki akasema kwenye uchumi kuna kitu
kinaitwa “economic paradoxes”, naona mnashangaa sana uongozi uliopita kulikuwa
na ufisadi, na rushwa na bado pesa ilikwepo
lakini sasa hivi hela hamna mnasikia majipu yametumbuliwa mengi.
Mawasiliano kwa namba 0656 859045 au barua pepe
petermmbaga29@gmail.com