Showing posts with label HISTORIA ILIOJEE!. Show all posts
Showing posts with label HISTORIA ILIOJEE!. Show all posts

Saturday, 15 October 2016

HISTORIA ILIOJEE: DEO FILIKUNJOMBE



Ni  historia iliojee tayari kwa aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Ludewa,  moja kati ya miiba iliyokuwa inachoma Serikali katika mijadala ya Bunge  japo ni mwanaCCM mwenzao, siku kama ya leo  ni kumbukumbu ya kifo chake alifariki dunia kwenye ajali ya helicopter iliyoanguka kwenye eneo la msitu wa mbuga ya Selous. Si mwingine ni ndugu Deogratius Filikunjombe “Deo”  mzaliwa wa wilaya ya  Njombe(sasa mkoa wa Njombe)  Machi 4, 1972.
Ndugu Deogratius Filikunjombe akiwa na abiria wengine wawili pamoja na rubani Kapteni William  Silaa, walikutwa wamekufa katika eneo la ajali  Oktoba 16, 2015.
Polisi walithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ya Chopa, chapa 5Y-DKK, iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Ludewa. Taarifa za awali zilitolewa na  mgombea ubunge jimbo la Ukonga kupitia CCM siku hiyo, Mh. Jerry Silaa, aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram sbaada ya tukio, alifafanua kuwa baba yake Kapteni  Silaa ndiye alikuwa rubani na kwamba mawasiliano kutoka eneo la tukio, yalikuwa magumu licha ya juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na vyombo husika kutafuta eneo la ajali.



Ndugu Filikunjombe, akifahamika kama Deo Haule  aliitumikia taaluma yake ya mawasiliano ya umma  akiwa Kampala, Uganda akiripotia kituo cha ITV/Radio One..
Ameondoka lakini atakumbukwa kwenye bunge la kumi kwa kuchachafya vilivyo, pasipo kuwa na uchama kwenye mambo ya kitaifa, hasa alipokuwa akizungumzia “issue” ya ESCROW. Kwa vijana wa kileo alibeba karisma ya “kutotekwa” na uchama kwenye kutetea maslahi ya wananchi kama viongozi wengine, hivyo anatujenga kwa “ombwe” la kimaslahi ya kivyama “lisituoe”  Kitaalamu alikuwa ni msomi wa shahada ya Mawasiliano ya Umma aliyotunukiwa Chuo Kikuu cha Makerere nchini, Uganda.  Alijiunga na Jeshi la Polisi na kufanya kazi kwa mwaka mmoja kisha akaacha kazi , baadaye  alipangiwa kitengo cha Habari makao makuu ya Polisi na kufanya kazi kwa mwaka mmoja. Bada ya Polisi alijiunga na World Vision kama  Afisa Mawasiliano(Communication/Information Officer)  na kufanya kazi kwa miaka kama minne hivi akiwa Makao makuu Arusha na baadae akahamishiwa tawi la Dar es salaam.
Alipotoka World Vision akajiunga na MKURABITA,  ambapo alifanya kazi kwa muda usiozidi miaka miwili akaacha.
Baada ya kuacha MKURABITA, akafungua duka lake la “electronics” lipo Benjamin Mkapa Tower, opposite na Posta Mpya ghorofa ya kwanza. Baadaye akaafungua vituo vyake vya kuuzia mafuta Ludewa na ndipo akaanza harakati za kuingia kwenye siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010. Inasemekana alikuwa hapendelei  kuwa mwanasiasa, japo baba yake alikuwa mkongwe wa TANU.
Mpaka anafariki ameacha mke na watoto wa tatu wa kiume.
Deo (kushoto) akiwa na mmoja wa rafiki zake  Bw. Zitto Kabwe enzi za uhai wake


Kwa vijana wa kileo alibeba karisma ya “kutotekwa” na uchama kwenye kutetea maslahi ya wananchi kama viongozi wengine, hivyo anatujenga kwa “ombwe” la kimaslahi ya kivyama “lisituoe”  bali siku kama ya leo ndiyo alitutoka!
Kwa sisi WAUNGWANA ni HISTORIA ILIOJEE tutamkumbuka!


Wednesday, 12 October 2016

HISTORIA ILIOJEE: BIBI TITI MOHAMED

Bibi Titi Mohamed

 Ni HISTORIA ILIOJEE! mwanamke jasiri, shujaa na mwenye msimamo, moja ya barabara kuu ndani ya jiji la Dar es Salaam, jina lake limo kwa heshima ya mchango wake mkubwa wa  kuleta uhuru wa Tanganyika.
Si mwingine ni Bibi Titi Mohamed,  mwanamama, aliyekuwa kiongozi  mmojawapo katika  harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, baadaye aliongoza Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), chama cha wanawake katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU), na baadaye akawa waziri wa wanawake na masuala ya kijamii katika serikali ya Mwalimu Nyerere.
Bi Titi  Mohamed alikuwa mwanamke wa Kiislamu aliyezaliwa jijini Dar es Salaam mnamo  mwaka 1926 na baba mfanyabiashara na mama mkulima. Alipata elimu ya shule za msingi pekee na alipofikisha  umri wa miaka 14 tu aliolewa na mume mzee.
Bi Titi Mohamed alipata nguvu  ya kuwa mwanaharakati   kupitia kipaji cha kuimba, enzi za ujana wake alikuwa mwimbaji mzuri wa kwasida na hivyo kuwa  kama mwimbaji kiongozi katika ngoma katika kikundi cha muziki na ngoma ambacho kilimwongozea uzoefu wa kuwa mbele ya umati.
Nguvu ya kushiriki katika majukumu ya uongozi na uhusiano ndani ya mitandao wanawake na mapambano ya kitaifa yallianza mwaka 1950, baada ya Vita Kuu ya II ya dunia, Tanganyika ikiwemo nchi  nyingine katika harakati za uzalendo zilikuwa zimeshika kasi. Mwaka 1954, TANU iliundwa chini ya uongozi wa mwalimu na  baadaye Rais Julius Nyerere. 
Bibi Titi na Mwalimu J.K Nyerere kwenye pozi enzi hizo
Muda si mrefu baadaye mwaka  1955, Bibi Titi alikasimishwa  kiti cha UWT, na ndani ya miezi mitatu ya uteuzi wake, walijiunga wanawake zaidi ya 5,000 kama wanachama wa TANU, na hivyo kwa mrengo huo wa  wanawake uliianzishwa na jukumu kubwa kwa mapambano ya uhuru na UWT kufanya kazi kubwa ya kukuza maadili  ya TANU kwa raia. Pia umoja wanawake ukapaza sauti moja katika mapambano dhidi ya ukoloni.
 Bibi Titi kupitia wanaharakati wanawake walikuwa na uwezo wa kutumia mitandao yao mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa kuongeza fedha kwa kiasi kikubwa kwaajili ya chama cha  TANU. Zaidi ya hayo, Bibi Titi akiwa na kipawa cha  usemaji, yeye mwenyewe, alihamasisha wanawake kupitia makundi ngoma na kusimamia viongozi wao kuunda nafasi kwa ajili ya kushughulikia wanachama na kuwasaidia, pia  makundi hayo yalikuwa wazi kwa wanawake wote waliotaka kujiunga, na kuishia kuwa mitandao yenye nguvu  kisiasa ajili ya kubadilishana taarifa,  tangazo la mikutano ya kampeni na maandamano.

Mwishowe mafanikio yaliingia  mwaka 1961,  kwa Tanganyika kupata Uhuru. 
Bibi Titi Mohamed bahati mbaya kisiasa  ilimpata mwaka 1965 wakati alipopoteza kiti chake cha ubunge. Mwaka 1967, yeye alijiuzulu kutoka uwaziri .
Baadaye alipata masaibu ya kisiasa  kwa kiasi kikubwa ilifanya kutoweka katika maisha ya umma na  baadaye   mnamo   Novemba 5, 2000,  Bibi Titi Mohamed pumzi yake ilirejea ilipotoka katika  hospitali ya Net Care huko Afrika Kusini.
HISTORIA ILIOJEE inajivunia Bibi Titi, mwanamama wa shoka, malkia wa nguvu  atakumbukwa kwa mengi,  heshima yake  ipo kwenye kutoa mwanga wa harakati za wanawake dhidi ya mfumo  mibovu  kwenye kila nyanja ya maisha,  kwetu sisi  WAUNGWANA ni HISTORIA ILIOJEEE!




Unakaribishwa kuacha comment yako hapo chini!

Saturday, 3 September 2016

HISTORIA ILIOJEE: NDUGU CLEOPA DAVID MSUYA



Ni HISTORIA ILIOJEEE, Mtanzania pekee aliyabahatika kuteuliwa  kwa kofia ya waziri mkuu na marais wawili tofauti, hapa namaanisha  Baba wa Taifa mwl. Julius  Kambarage Nyerere pamoja na  Rais wa awamu pili ndugu Alli Hassani Mwinyi,  si mwingine ni ndugu Cleopa David Msuya .
Mara ya kwanza ilikuwa ni siku 13 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1980 wa chama kimoja, ambapo kama kawaida mnapotoka uchaguzini, moja ya kazi za kwanza ya Rais ni kumtangaza Waziri Mkuu, na ndipo hapa November 07, 1980 Mwl. Julius Nyerere akamtangaza Cleopa Msuya kuwa Waziri mkuu. huyu ndiye ndugu Cleopa David Msuya aliyezaliwa novemba 4, 1931, huko wilayani Mwanga, tarafa ya Usangi katika kijiji cha Chomvu mkoani Kilimanjaro.
Ni kizazi cha wasomi wa Chuo Kikuu cha Makerere toka mwaka 1952 mpaka 1955,  ndugu Msuya  aliyeanza kwa utumishi wa  sekta ya umma, maendeleo ya vijiji toka mwaka 1956 hadi 1964. Kuanzia mwaka 1964 alihudumu kama katibu kiongozi kwenye wizara tofauti tofauti ikiwemo wizara ya maendeleo ya jamii na utamaduni kutoka mwaka 1964 hadi 1965, wizara ya makazi na maendeleo ya maji kati ya mwaka 1965 mpaka 1967, 1967 mpaka 1970 ilihudumu kwenye wizara ya uchumi na mipango na baadaye akahamishiwa wizara ya fedha toka mwaka 1970 hadi 1972.
Februari mwaka 1972 aliteuliwa kuwa waziri wa fedha mpaka mwaka 1975 aliula tena kuiongoza wizara ya viwanda na biashara  hadi mwaka 1983, alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa wa kuwa waziri mkuu.
Alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu na  Makamu wa pili wa Rais, ndugu Msuya hakumaliza awamu yote kwani  mnamo Februari 24, 1983 alibadilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Hayati Edward Sokoine ambaye naye hakumaliza awamu ile kwani alifariki mwaka mmoja tu baadaye yaani April 12, 1984.
Awamu  pili ndugu  Msuya aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu Desemba, 1994 alipoteuliwa na Rais Ali Hassani Mwinyi kupokea  nafasi ya John Malecela ambaye alijiuzulu siku mbili kabla ya uteuzi huu wakati kikao cha NEC-CCM, kikiendelea. Hivyo kutokana na katiba kuruhusu akawa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais wa jamhuri ya Muungano.
 Hapo nyuma mnamo mwaka 1992, nchi yetu iliingia katika mageuzi makubwa ya mfumo wa kisiasa pale ilipoamua kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mabadiliko haya yalisababisha Katiba ya nchi ifanyiwe mabadiliko ili kuruhusu mfumo huu wa demokrasia ya vyama vingi ufanye kazi nchini ambapo nafasi mbalimbali za uongozi pia ziliguswa na mabadiliko hayo hivyo mwaka 1994, kufuatia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kuruhusiwa nchini ilijitokeza haja ya kuifanyia mabadiliko nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili iweze kukidhi mageuzi haya ya kisiasa. Ilionekana kwamba katika mfumo huu mpya wa demokrasia ya vyama vingi si rahisi tena kuwa na Makamu wa Rais wawili kama ilivyokuwa wakati wa mfumo wa demokrasia ya chama kimoja hivyo ndugu Cleopa mwana  David  ndiye  aliyemalizia rojo ya tamu na shubiri ya kuwa na vyeo viwili vikubwa kwa wakati mmoja.
Nafasi alizokuwa nazo aliziacha kwenye uchaguzi mpya wa kihistoria wa vyama vingi uliofanyika kwa mara ya kwanza mwa 1995, na baadaye kuteuliwa kuwemo kwenye bunge maalum la katiba nafasi aliyodumu nayo hadi kustaafu mwaka 2000. Alipata nafasi ya kuwa nwenyekiti wa kilimanjaro gvt forum mwaka 2006.
Hadi kustaafu kwake ameeendelea kuwa kada mwaminifu wa chama cha mapinduzi hadi hii leo.

Ni HISTORIA ILIOJEE kwetu sisi WAUNGWANA  kumgusia  ndugu Cleopa Msuya ambaye kipekee mpaka sasa ndiye Waziri Mkuu wa kwanza Tanzania kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mtindo wa sasa kuthibitishwa na Bunge na pia kushika vye vikubwa awamu mbili  yaani   Waziri mkuu kikiongozana na Makamu wa Pili wa Rais wa  Jamhuri na baadaye Waziri  Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa wakati mmoja kwasababu ni  HISTORIA ILIOJEEE!!!!