Mamlaka
ya wawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wafanyabiashara wenye leseni za
kuingiza simu nchini, zinazotolewa na mamlaka hiyo, kutekeleza maagizo
yaliyotolewa na Kampuni ya Samsung ya kurejesha simu za kisasa za Samsung
Galaxy Note 7 baada ya kubainika zina matatizo ya betri. Akizungumza Dar es
Salaam Ijumaa hii na gazeti la habari leo, meneja mawasiliano wa TCRA, Innocent
Mungy, alisema ni vyema mawakala hao wakatekeleza maagizo hayo, kwani simu hizo
ni hatari kuendelea kutumika.
“Simu
hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri na mara mbili sasa
imelipuka, hakuna faida ya mtu kuendelea kuitumia unaweza ukasababisha hatari
kubwa, inapolipuka inaweza kukuondoa mikono, inaweza kulipua nyumba na matatizo
mengine tunawataka wenye simu hizo kuziridisha haraka,” alisema Mungy.
“Taarifa
tulizonazo haijaingia sana hapa nchini lakini wapo walioletewa kama zawadi
kutoka nje ya nchi nawaomba warudishe huko kuepuka matatizo yanayoweza
kujitokeza,” aliongeza.
Samsung
iliwataka watu waliokuwa wamenunua jumla ya simu milioni 2.5 mwezi Septemba
mwaka huu, kuzirejesha madukani baada ya wateja wengi kulalamika kwamba betri
za simu hizo zilikuwa zinalipuka. Katika hatua nyingine, wiki iliyopita,
Kampuni hiyo ya Samsung ya Korea Kusini ilitangaza kuwa imesitisha utengenezaji
wa simu aina ya Galaxy Note 7.
Aidha
Mungy aliwataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo kuzizima na
kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua ili kuepusha hatari ambayo
tayari Samsung wameshaitoa.
No comments:
Post a Comment