Kansela Merkel
akikamilisha ziara yake Afrika ameahidi kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi wa
Ethiopia kuhusu namna ya kukabiliana na waandamanaji. Ametaka waandamanaji
wapewe uhuru wa kuandamana na uhuru kwa wapinzani.
Waziri mkuu wa
Ethiopia Hailemariam Desalegn amesema serikali yake inataka kufanya mageuzi ya
mfumo wa uchaguzi, ambao kwa muda mrefu umeutenga upinzani na kuchangia kutokea
kwa maandamano mabaya ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa. Haya yanajiri wakati
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akimaliza ziara yake nchini humo ambapo
amesema waandamanaji waruhusiwe kuandamana.
Waziri mkuu wa
Ethiopia Hailemariam Desalegn amewaambia wanahabari kuwa “kufuatia mfumo uliopo
sasa wa uchaguzi nchini humo, asilimia 51 ya kura inatosha kutwaa ushindi wa
viti vyote". Na sasa serikali yake inataka kufanya marekebisho ili
kuhakikisha mfumo huo unabadilishwa ili watu wote wakiwemo wapinzani
wawakilishwe bungeni.
Chini ya mfumo uliopo
sasa, muungano wa Hailemariam ambao ndio unatawala, ulishinda viti vyote 546
vya ubunge katika uchaguzi mkuu, uliofanywa mwaka jana. Hii hapa kauli ya
Hailemariam kuhusu suala, la demokrasia na usalama nchini mwake."Ethiopia
imejitolea kukuza demokrasia.Ethiopia imejitolea kuwa na demokrasia ya vyama
vingi kulingana na katiba yetu. na Ethiopia imejitolea kuhakikisha haki za
binadamu zinalindwa. Lakini Ethiopia pia inapinga ghasia ya misimamo mikali au
makundi yanayojihami kwa fujo".
Hailemariam aliyasema
hayo baada ya kukutana na mgeni wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,
akimaliza ziara yake ya siku tatu barani Afrika, ambapo amesema demokrasia
iliyoimarika inahitaji kuwepo na upinzani pamoja na uhuru wa vyombo vya habari.
Ameitaka Ethiopia kuwapa uhuru waandamanaji bila ya ukandamizaji wa aina
yoyote. Kando na kuhimiza serikali kufanya mazungumzo na upinzani, Merkel pia
ameahidi kuwa, nchi yake itatoa mafunzo kwa maafisa wa polisi wa Ethiopia
kuhusu namna ya kukabiliana na waandamanaji.
Akiwa Ethiopia,
Kansela Merkel amemwambia mwenyeji wake Waziri Mkuu Desalegn kuwa waandamanaji
waruhusiwe kuandamana na kuwa hatua yoyote ya vyombo vya usalama iwe kulingana
na sheria. Kadhalika amesema wanaharakati wa upinzani na watetezi wa haki za
kibinadamu wanapaswa kuwa na uhuru wa kutekeleza majukumu yao. Lakini Waziri
Mkuu Hailemariam amepinga madai kuwa maafisa wa polisi walitumia mbinu za fujo
dhidi ya waandamanaji, na kuahidi kuwa serikali yake itachunguza visa hivyo.
Wiki iliyopita, zaidi
ya watu 50 waliuawa kwenye mkanyagano baada ya polisi kujaribu kuwatawanya
waandamanaji. Hali iliyosababisha kuongezeka kwa maandamano zaidi, na
kulazimisha serikali kutangaza hali ya hatari nchini humo mwote.
Ethiopia imekumbwa na
maandamano ya miezi kadhaa ambapo waandamanaji wanashinikiza kupatikana kwa
uhuru wa kisiasa na haki ya kumiliki ardhi, huku wakilaumu serikali kwa
kuendeleza utawala wa kimabavu.
Katika kipindi cha
mwaka mmoja uliopita, watu 400 wamekufa nchini Ethiopia kutokana na maandamano
hayo dhidi ya serikali. Hayo yamesemwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu
pamoja na wanaharakati wa upinzani.
Jumatatu wiki hii,
rais wa Ethiopia alitangaza bungeni kuwa sheria za uchaguzi zitafanyiwa
marekebisho ili kuruhusu vyama vingi vya kisiasa na kuwapa nafasi wapinzani.
Hata hivyo, matumizi ya mtandao yangali yamezimwa nchini humo, baada ya
maandamano kuzidi kwa muda wa wiki moja ambapo pia waandamanaji walifanya
uharibifu katika biashara na afisi za ubalozi wa nchi zinazofikiriwa
kushirikiana na serikali.
Marekani na mataifa
mengine yameitaka serikali ya Ethiopia kujizuia katika kukabiliana na
waandamanaji huku maafisa wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wakitaka
uchunguzi huru ufanywe kuhusu matukio hayo katika eneo la Oromia.
Merkel amekamilisha
ziara yake ya siku tatu katika nchi za Mali, Niger na Ethiopia yenye lengo la
kuhimiza uimarishaji wa usalama ili kupunguza wimbi la wakimbizi. Ethiopia
ni mojawapo ya nchi inayowahifadhi wakimbizi wengi duniani. Mamia ya maelfu ya
wakimbizi hao wakitoka Somalia, Sudan Kusini na kwingineko. Sawa na Ujerumani
ambayo.
Merkel pia inakumbwa
na mzigo wa wakimbizi kwa sasa, ambapo takriban wakimbizi mioni moja waliingia
Ujerumani tangu mwaka jana pekee.pia amefungua rasmi jingo jipya la Muungano wa
Afrika ambalo pia litakuwa la baraza la amani na usalama. Jengo hilo lililopo
Addis Ababa limejengwa kwa ufadhili wa yuro milioni 27 kutoka Ujerumani.
Chanzo: DW
.
No comments:
Post a Comment